Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Simba SC watacheza dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza Pamba FC katika mchezo wa hatua ya Robo Fainali.
Simba SC iliyotinga hatua ya Robo Fainali kwa kishondo kikubwa cha kuitandika Ruvu Shooting mabao 7-0, imemfahamu mpinzani wake kwenye michuano baada ya kupangwa kwa Ratiba mapema hii leo Jumatatu (Februari 21)katika Studio za wadhamini wakuu Kampuni ya Azam Media.
Wakati Simba ikipangwa kukutana dhidi ya Pamba FC, Watani zao wa Jadi Young Africans wamepangwa kukutana na Geita Gold FC, huku Azam FC ikipangwa dhidi ya Polisi Tanzania.
Mchezo mwingine wa Robo Fainali utakua kati ya Kagera Sugar FC dhidi ya Coastal Union ambayo itakua nyumbani Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Wakati huo huo TFF kwa kushirikiana na Wadhamini wa michuano hiyo Azam Media, wametangaza Ratiba ya Michezo ya Nusu Fainali, ambapo Mshindi wa mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Pamba FC atakutana na Mshindi wa Mchezo kati ya Young Africans dhidi ya Geita Gold.
Mchezo mwingine wa Nusu Fainali utakua kati ya Mshindi wa mchezo wa Azam FC dhidi ya Polisi Tanzania ambaye atacheza na Mshindi wa mchezo kati ya Coastal Union dhidi ya Kagera Sugar.
Michezo ya Robo Fainali imepangwa kuchezwa kati ya April 08 hadi 13.