Kukamilika kwa mradi wa kupeleka umeme kwenye Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Geita Gold Mining (GGM) kutaliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupata kiasi cha shilingi bilioni 5 kwa mwezi zitakazotokana na mauzo ya umeme.

Hayo yamebanika leo Februari 21, 2022 wakati wa shughuli ya utiaji saini mkataba wa mauziano ya nishati ya umeme baina ya TANESCO na GGM.

Akiongea katika zoezi hilo Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande amesema kuanza kwa biashara hiyo kutaiwezesha TANESCO kuongeza mapato yatakayosaidia kuboresha huduma mbalimbali kwa wateja wao.

“Maana ya pili tutapunguza uzalishaji wa hewa chakafu ya dizeli, lakini pia kuongeza ufanisi wa kazi zao GGM kwa maana ya gharama za uzalishaji zitapungua,” alisema Maharage.

Aliongeza kuwa, hatua hiyo kubwa na muhimu ya GGM kuunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa imefikiwa baada ya miaka zaidi ya ishirini tangu kuanzishwa kwa kampuni ya GGM.

Kufanikiwa kwa jambo hilo kumetokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na TANESCO katika kuimarisha upatikanaji wa umeme ndani ya Mkoa wa Geita kwa kujenga kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mpomvu chenye uwezo wa megawati 90.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa GGM, Simon Shayo amesema GGM watajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme kutoka kilovolti 33 hadi 11 ambazo zitatumika kwa matumizi ya mgodi.

“Kwetu sisi tunapunguza gharama za uzalishaji wa umeme tunao utumia kwa maana kwa kuacha kutumia mafuta lakini pia kutunza mazingira, Dunia sasa inatoka kwenye  matumizi ya mafuta ambayo yanazalisha hewa ya ukaa,” amesema Shayo.

Kampuni ya GGM Kwa sasa inatumia senti 19 dola za kimarekani kuzalisha umeme kwa unit moja kwa kutumia mafuta, ambapo mradi huo ukikamilika na kuunganishwa na gridi watatumia senti 9  za kimarekani kwa unit moja kupata umeme.

Mradi huo wa kupeleka umeme GGM unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu,  ambapo utajumuisha njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilometa 6 na kituo cha kupoza umeme cha GGM.

Mtibwa Sugar yamjibu Haji Manara
Simba SC, Young Africans zachonganishwa ASFC