Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kinaondoka leo mjini Niamey-Niger kuelekea Morocco, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Mzunguuko wa tatu wa Hatua ya ‘Kundi D’ dhidi ya RS Berkane.
Simba SC ilikua na kibarua kigumu jana Jumapili (Februari 20) mjini Niamey, cha kuikabili US Gendermarie na kuambulia sare ya 1-1, iliyoifanya kufikisha alama 4 katika msimamo wa ‘Kundi D’.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amethibitisha kuwa safari yao ya kuelekea Morocco, itakua rasmi leo Jumatatu (Februari 21), wakipitia nchini Uturuki.
Ahmed amesema kikosi chao kitaweka Kambi nchini Morocco kujiandaa na mchezo dhidi ya RS Berkane, huku wakiamini muda wa siku nne watakazokuwa huko utawatosha kuwa na maandalizi mazuri.
“Tukiwa Morocco tutaweka kambi ya siku kadhaa, tunaamini tutajiandaa vizuri kabla ya kukutana na wapinzni wetu Jumamosi (Februari 27), lengo la Simba SC ni kuendelea kuongoza msimamo wa Kundi D, tunaamini hilo linawezekana.” Amesema Ahmed Ally
Simba SC tayari imeshacheza michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Hatua ya Kundi D, wakishinda dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast mabao 3-1 na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya US Gendermarie ya Niger.