Kikosi cha KMC FC kitaingia kambini Kesho Jumanne (Februari 22), kwa ajili ya kujiandaa na Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo kitakutana na Polisi Tanzania Jumamosi ya (Februali 26).
KMC FC wamejipanga kuanza kambi ya kuwakabili Maafande hao wa Jeshi la Polisi, baada ya kuiadhibu Dodoma Jiji FC mabao 2-0 jana Jumapili (Februari 20), Uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, kikosi cha KMC FC leo Jumatatu (Februari 21) kimepewa mapumziko na kesho Jumanne (Februari 22), kitaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa KMC FC Christina Mwagala amesema kikosi chao kinachonolewa na Kocha Mkuu Thiery Hitimana kimejipanga kufanya vizuri kwenye michezo ya mzunguko wa pili ili kuzidi kujiimarisha katika nafasi ya msimamo wa Ligi kuu na hivyo kumaliza ligi kwenye nafasi ambayo klabu ilijiwekea malengo ambayo ni nafasi tatu za juu.
“Tumepata matokeo mazuri ambayo tuliyahitaji kwa namna yake katika mchezo huo, ulikuwa mchezo mgumu lakini ubora wa wachezaji tulionao ndio uliamua matokeo ya mchezo wetu wa jana, hivyo tunawapongeza kwa kazi kubwa ambayo waliifanya ya kuleta furaha kwa mashabiki zetu ambao kila siku wamekuwa mstari wa mbele kuisapoti Timu.”
“Kitu kikubwa ambacho tulikifanya ni kutumia nafasi vizuri ambazo tulizipata, wachezajii na Benchi la ufundi lilijipanga vema kwenye mchezo huo kwasababu tulifahamu tunakutana na timu ambayo imetoka kupoteza hivyo nilazima kucheza kwa tahadhari na umakini mkubwa, tunamshukuru Mungu tulifanikiwa na kuondoka na alama tatu muhimu na magoli mawili ambayo yalifungwa na Awesu Awesu pamoja na Hassan Kabunda.” Amesema Christina Mwagala
Hadi sasa KMC FC imecheza michezo 15 ikiwa kwenye nafasi ya tisa 9 ikiwa na alama 19, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo kati ya michezo hiyo imeshinda michezo Minne , sare Saba na kupoteza michezo Minne.