Serikali imetoa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia kwa wakufunzi wote 2,300 kutoka Vyuo vya Ualimu vya Serikali yote 35.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo Februari 21, 2022 wakati wa hafla ya ugawaji wa kompyuta kwa vyuo vya ualimu awamu ya tatu iliyofanyika Jijini Dodoma.

Waziri Mkenda amesema kuwa wizara imekwishagawa vifaa vya TEHAMA ikiwa ni Kompyuta za Mezani (Desktop) 1,120, Kompyuta za mkononi au Kompyuta Mpakato (laptop) 113, na Projekta 186.

Vifaa hivyo viligawiwa kwa Vyuo vyote 35 vya Ualimu, ikiwa ni nyongeza ili kukidhi mahitaji jambo litakalosaidia kupunguza uwiano wa matumizi ya kompyuta kwa Wanachuo kutoka Wanachuo 28 kwa Kompyuta 1 (28 :1) hadi kufikia Wanachuo 2 kwa Kompyuta 1 (2 :1) vyuoni.

“Kwa matumizi ya vifaa na mifumo hiyo ya TEHAMA iliyoboreshwa inahitaji pia kuwepo kwa Mtandao imara, hivyo, Wizara itaviunganisha Vyuo vyote vya ualimu katika Mkongo wa Taifa ili kuhakikisha kuwa Vyuo vinaweza kupata mtandao imara utakaowawezesha Wakufunzi na wanachuo kutumia ufundishaji na ujifunzaji kwa ufanisi.” Amesema Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa kwa mwaka huu wizara inatarajia kuunganisha Vyuo 15 vya Ualimu katika Mkongo wa Taifa baada ya Wizara kuwakabidhi wakandarasi wawili (BM Telecommunication na SoftNET Solution).

Prof Mkenda amesema kuwa Mgao wa kompyuta hizo umezingatia uwiano kati wanachuo na vifaa vilivyopo katika Vyuo kwa sasa.

“Jumla ya Kompyuta 300 zimegaiwa kwa Vyuo 13, Vyuo 4 vimepata Kompyuta 30 na Vyuo 9 vimepata Kompyuta 20. Aidha, Vyuo vyote 35 vitapatiwa Kompyuta Mpakato 1 kwa ajili ya kusaidia idara mbalimbali vyuoni,” amesema Prof, Mkenda.

Wizara inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Vyuo mbalimbali nchini ikiwemo ukamilishaji wa Chuo cha Kabanga, Ujenzi wa vyuo vipya vya Sumbawanga, Dakawa, Mhonda na Ngorongoro. Aidha, Ukarabati na ujenzi wa baadhi ya miundombinu katika vyuo vya Morogoro, Mpwapwa, Tukuyu, Kasulu, Butimba na Patandi nao unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha 2021/2022.

Wamachinga watakiwa kutumia fursa
Simba SC yamuwinda Arno Buitenweg