Uongozi wa Klabu ya Young Africans umewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuelekea mchezo wa Mazunguuko wa 15 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kesho Jumatano (Februari 23) dhidi ya Mtibwa Sugar.

Young Africans imesafiri hadi Wilayani Mvomero yalipo maskani makuu ya Mtibwa Sugar, tayari kwa mchezo huo utakaopigwa katika Uwanja wa Manungu Complex kuanzia mishale ya saa kumi jioni.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema Idara zote za klabu hiyo zimejiandaa kuelekea mchezo huo, na wanaamini alama tatu muhimu zitakwenda Jangwani.

Amesema kuna mambo mengi ambayo wameyaona na wanayasikia kuhusu mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini mpaka sasa wamejithibitishia hakuna lolote ambalo litawaathiri kwenye mipango yao ya kuhakikisha wanaendelea kuwa klabu pekee ambayo haijafungwa kwenye Ligi Kuu msimu huu.

“Tuwaambie ndugu zetu Mtibwa Sugar kuwa kukamia sio kuzuri, wasitukamie kwa sababu mchezo wa soka unachezwa hadharani na unaonekana na kila shabiki wa mchezo huu.”

“Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo huu, wasijidanganye sana kuhusu porojo za watu zinazopigwa kwenye mitandao ya kijamii, Young Africans tupo vizuri, tumejiandaa kucheza soka safi ambalo litatuwezesha kushinda kwenye Uwanja wao wa Manungu Complex kesho Jumatano.” amesema Bumbuli.

Kikosi cha Young Africans iliwasili jana Jumatatu (Februari 21) Mjini Morogoro kikitokea jijini Dar es salaam, leo Jumanne (Februari 22) kilifanya mazoezi ya mwisho mjini humo kabla ya kuanza safari ya kuelekea Manungu, Turiani Wilayani Mvomero yalipo makao makuu ya wapinzani wao.

Young Africans ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 36 baada ya kucheza michezo 14, huku Mabingwa watetezi Simba SC wakiwa kwenye nafasi ya Pili kwa kumiliki alama 31 zilizotokana na michezo 15 waliocheza.

Mtibwa Sugar itakayocheza na Young Africans kesho Jumatano (Februari 23) kwenye Uwanja wa Manungu Complex, ipo nafasi ya nafasi 15 ikiwa na alama 12 kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Young Africans yachekelea kuikwepa Pamba FC
Bonde la mto Nile fahari ya Afrika