Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison huenda asiondoke Simba SC mwishoni mwa msimu huu, kufutia mfadhili wa zamani wa klabu hiyo Azim Dewji kumkingia kifua.

Mkataba wa Morrison na Simba SC unatarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa hakuna taratibu zozote za kuanza mazungumzo baina ya pande hizo mbili hadi sasa.

Hali hiyo imeifanya klabu ya Young Africans kuanza kutajwa kuwa kwenye mpango wa kumuwani tena Morrison, ambaye aliachana na klabu hiyo mwanzoni mwa msimu uliopita baada ya mkataba wake wa miezi Sita kufikia kikomo.

Azim Dewji amesema Morrison ni mchezaji mzuri ambaye kila timu hapa nchini inatamani kuwa naye, lakini kinachomuangusha mchezaji huyo kutoka Ghana ni changamoto ya kinidhamu.

“Morrison ni mchezaji mzuri na kama unavyoona juzi ametufungia bao muhimu ugenini dhidi ya timu ya Niger (US Gendarmerie) ambalo limetupatia pointi na kutufanya tuongoze kundi jambo ambalo ni zuri,” amesema Azim na kuongeza;

“Napenda kuona akiendelea kuichezea Simba kwani ana kipaji na uwezo mkubwa ingawa lazima itafutwe njia ya kumsaidia nayo ni kupatiwa mtaalam wa kisaikolojia ambaye atamuweka sawa na kumfanya atulie na awe na nidhamu ya hali ya juu. Akitulia anatoa mchango mkubwa sana kwa timu.”

Azim amesema hana shaka na kiwango na kipaji cha Morrison lakini masuala ya utovu wa nidhamu yatamrudisha nyuma hivyo mchezaji huyo anayemudu vyema kucheza nafasi ya winga na mshambuliaji wa kati anapaswa kubadilika na kuwa na tabia njema.

Kauli hiyo ya Azim ni kama inafuta ila aliyoitoa mwaka jana pale alipolishauri Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ kumrudisha mchezaji huyo nchini Ghana baada ya kuziingiza kwenye mgogoro wa kiusajili, Simba na Young Africans.

“Kwa upande wangu naona ni kitu chepesi tu. TFF wamrudishe huyo mchezaji kwa sababu mbili muhimu. Huyu mchezaji akichukua maamuzi ya kuchezea Yanga hawawezi kumchezesha na kwa ajili watakuwa hamuamini. Na akija upande wa Simba huyu kijana hana nidhamu sasa ataanza kuharibu wachezaji wengine,” alinukuliwa Azim.

Hivi karibuni, Morrison alisimamishwa na Simba kwa muda usiojulikana baada ya kudaiwa kuondoka kambini bila ruhusa ingawa baadaye alirudishwa kundini baada ya klabu hiyo kusema kuwa aliandika barua ya kuomba msamaha.

Ahmed Ally aipongeza RS Berkane
Haji Manara aishangaa Simba SC