Mwenyekiti wa Klabu ya Young Africans Mshindo Mbette Msolla ameibuka kwa mara ya kwanza msimu huu na kutoa nasaha kwa Benchi la Ufundi na Wachezaji wa klabu hiyo, kufuatia mwenendo wao katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 41, huku ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa Ubingwa msimu huu 2021/22, baada ya kutoka kapa kwa misimu minne mfululizo huku wakiwashuhudia watani zao Simba SC wakilitawala Soka la Bongo.

Mshindo Msolla amewataka wachezaji wa klabu hiyo kuendelea kuipigania klabu yao bila kuchoka, ili kufikia lengo la kurejesha heshima ya ubingwa wa Tanzania Bara, ambao kwa mara ya mwisho waliupata msimu wa 2016/17.

Amesema mpaka sasa ameridhishwa na kila mchezaji aliyepata nafasi ya kuipigania Young Africans na matumaini yake ni kuona moto waliouwasha tangu kuanza kwa msimu huu hauzimwi hadi mwisho.

“Ninawapongeza wachezaji wetu kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya, ninaamini mambo yanaendelea kuwa mazuri na yatakua mazuri mwishoni mwa msimu huu.”

“Lengo letu ni kutwaa ubingwa msimu huu, kwa kikosi tulichonacho ninaamini hakuna kitakachoshindikana zaidi ya kurejesha heshima yetu ya kuwa mabingwa katika nchi hii.”

“Tunaongoza ligi kwa ubora wake, anayetufuatia tumemuacha kwa alama nane na pia tumemzidi magoli 11, huu sio mtaji mdogo ni mkubwa sana katika soka la ushindani.”

“Ninawaomba sana Benchi la Ufundi na Wachezaji, tusimbweteke na mafanikio haya, kwa hiyo tuendelee kuongeza zaidi msukumo na kazi ya kujituma uwanjani, kwa hiyo ninachowasihi yoyote ambaye atakayepata nafasi apambanie ushindi kwa ajili yetu sote.” amesema Mshindo Msolla.

Young Africans iliichapa Kagera Sugar mabao 3-0 siku ya Jumapili (Februari 27), hatua ambayo imeendeleza rekodi ya kutokupoteza mchezo wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22.

Aiba simu za polisi na kusema Shetani alimpitia
Franco Pablo: Hatuna muda wa kupumzika