Shughuli katika Mahakama za Thika nchini Kenya zilisitishwa asubuhi ya Jumatano, Machi 2, 2022, kufuatia hofu ya ugaidi na Mahakama hiyo kufungwa kwa muda.

Katibu wa Chama cha Mawakili Kenya, Stephen Mbugua, wa tawi la Thika amesema kikosi cha usalama kilitumwa katika majengo hayo na kuwa mawakili na yeyote anayetafuta au kutoa huduma katika mahakama hizo walihamishwa huku hatua za tahadhari zikichukuliwa.

Mahakama ya Thika

Haya yanajiri baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Marekani (FAA) kuwaonya Wakenya wanaosafiri angani kuhusu uwezekano wa shambulio kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Al Shabaab lakini Mamlaka ilithibitisha kuwa kundi hilo la kigaidi bado ni tishio katika maeneo yenye watu wengi kama vile anga ya Kenya.

“Silaha kama hizo zinaweza kulenga ndege, ikijumuisha wakati wa kupaa na kutua au kulenga viwanja vya ndege zikiwa pia ardhini,” ushauri wao ulisema.

Zaidi ya hayo, serikali ya Ufaransa, kupitia kwa ubalozi wake, pia ilikuwa imetoa tahadhari kwa Kenya kuhusu shambulio linalowalenga wageni nchini humo na kuwaonya raia wake kujiepusha na maeneo ya umma ambayo yalionekana kuwa yalilengwa.

Maeneo ambayo yanakumbwa na shambulio ni pamoja na vituo vya biashara, hoteli, vituo vya starehe na migahawa na kati ya maeneo mengine ambayo watu hurundikana jijini Nairobi.

Serikali ya Ufaransa iliwataka raia wake kupiga nambari za dharura za ubalozi iwapo watavamiwa au kuwasiliana na mamlaka ya Kenya.

Ripoti hizo, hata hivyo, zilifutiliwa mbali na msemaji wa polisi Bruno Shioso ambaye alisema kuwa walikuwa bado hawajapokea taarifa zozote kuhusu shambulizi linalopangwa kutekelezwa.

Mtoto wa Museven aunga mkono Uvamizi wa Urusi kwa Ukraine
Marekani yatoa mapipa milioni 30 ya mafuta kunusuru ulimwengu