Serikali kupitia Wizara ya afya imetoa wito kwa wawekezaji wa nje kuwekeza nchini katika kutengeneza vyandarua vyenye dawa kwa teknolojia ya kisasa (New Generation Nets) kwa kusaidiana na wawekezaji wa ndani hatua inayotajwa kuwa itasaidia kubadilishana ujuzi na kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya Malaria.

Hayo yamesemwa leo tarehe 2 Machi, 2022 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipokutana na kufanya mazungumzo na Joy Phumaphi ambaye ni Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Umoja wa Marais wa Afrika katika mapambano dhidi ya Malaria (ALMA) katika ofisi za Wizara zilizoko Mtumba jijini Dodoma.

Waziri Ummy Mwalimu akizungumza na Joy Phumaphi katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba

Katika mazungumzo hayo ambayo yalilenga kuona namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Malaria, Waziri Ummy amemwambia Joy kuwa hatua hiyo ya uzalishaji wa vyandarua vyenye dawa vitakavyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa itasaidia kukabiliana na usugu wa mbu dhidi ya dawa aina na Paleto ambayo inatumika kwenye vyandarua hivi sasa.

Picha ya pamoja kati ya watendaji wa ALMA na Watendaji wa wizara ya afya

Pamoja na mengine Waziri Ummy amemwambia Joy kuwa Rais, Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanzishwa kwa baraza la kutokomeza Malaria ikiwa ni mkakati mmojawapo wa kukabiliana na Malaria ambapo uzinduzi wake utafanyika katika kilele cha siku ya maadhimisho ya Malaria duniani tarehe 25 Aprili 2022.

Kwa upande wake Joy ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo katika kutekeleza afua mbalimbali zinazoratibiwa na taasisi hizo na kumuahidi Waziri kuwa ALMA itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na sekta ya afya kwa ujumla ili kukabiliana na ugonjwa wa Malaria ambao bado unaendelea kuwa tishio kwa nchi nyingi za kiafrika.

UN yatuma ujumbe kwa Rais Putin
Rais Samia ateta na Viongozi wa dini