Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin, anaamini kurejea kwa baadhi ya wachezaji wake katika kikosi, kutamsaidia kufanya vizuri kwenye michezo inayomkabili kwa sasa.

Simba SC inatarajia kushuka tena dimbani kesho Jumatatu (Machi 07) kucheza mchezo wa Mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC, huku ikikabiliwa na mchezo mwingine wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco Machi 13.

Kocha Pablo amesema kurejea kwa viungo wake Rally Bwalya na Mzamiru Yassin kumeongeza nguvu na ari ya kufanya vizuri zaidi katika ratiba yao ngumu.

Bwalya ambaye amekuwa akitumika kucheza pacha kwenye kiungo cha timu hiyo na Clatous Chama hakuwepo katika timu hiyo kutokana na matatizo ya kifamilia.

“Tumekuwa na ratiba ya michezo mitatu migumu na muhimu dhidi ya Biashara United ambao tayari tumeshaumaliza kwa ushindi wa 3-0, Dodoma Jiji tutakaocheza kesho Jumatatu na RS Berkane utakaotukabili mwishoni mwa juma lijalo, kwa kuwa michezo hii ni ya mfululizo, tunahitaji kuwa na kikosi chetu kamili na wachezaji wote muhimu.”

“Nafurahi kuona tayari Mzamiru na Bwalya wakirejea kujiunga na wenzao baada ya kushindwa kusafiri nasi kwenye Kombe la Shirikisho, katika kipindi ambacho tunakabiliwa na majeruhi kurejea kwao ni wazi kumetuongezea nguvu ya kufanya vizuri zaidi.” Amesema Pablo.

Kiungo Mzamiru Yassin alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC juzi Ijumaa (Machi 04) kilichoikabili Biashara United Mara Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, huku akifunga bao la pili kati ya mabao matatu yaliyowapa alama tatu muhimu.

Kapombe kuikosa Dodoma Jiji FC
Kisinda aichimba mkwara Simba SC