Kocha Mkuu wa timu ya Polisi Tanzania, Malale Hamsini ameweka wazi kuwa sababu kubwa ya ushindi wao dhidi ya Azam FC juzi Jumamosi (Machi 05) ni ubora mkubwa aliokuwa nao Mlinda Lango wao, Metacha Mnata katika kuokoa hatari zilizoelekezwa Kangoni kwao.

Polisi Tanzania iliibuka na ushindi wa bao 1-0, katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, hali ambayo ilikua tofauti na ilivyotarajiwa na wadau wengi wa soka, kutokana na ubora wa Azam FC hasa wanapocheza nyumbani kwao.

Kocha Malale amesema uwezo wa Metacha ndio ulikua chachu ya mafanikio ya kuokota alama tatu muhimu katika mchezo huo, huku umakini wa mchezaji mmoja mmoja ukiongeza ari ya kupambana bila kuchoka ndani ya dakika 90.

“Ulikuwa mchezo mzuri na mgumu kwetu hususan kwa kuwa tulikuwa na wachezaji wengi ambao walikuwa majeruhi, lakini jambo la muhimu ni kuwa tumefanikiwa kupata pointi tatu muhimu.”

“Pia napenda kumpongeza kipa wangu Metacha Mnata ambaye ni wazi alikuwa kwenye kiwango bora Jumamosi, na naweza kusema bila yeye ingekuwa vigumu kupata ushindi.” amesema Malale Hamsini

Ushindi wa bao 1-0 umeifanya Polisi Tanzania kufikisha alama 22 zinazoiweka katika nafasi ya 07 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Azam FC ikiwa nafasi ya 04 kwa kumiliki alama 25.

DP Ruto: Nitamrejesha Miguna Nyumbani nikiwa Rais
Ummy Mwalimu: Afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali