Nahodha na Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania, Mbwana Samatta na mamia ya watu maarufu wamejitokeza kuchangia timu ya Taifa ya Wanawake ya Twiga Stars katika kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani kupitia Tamasha la The Orange Concert leo Machi 8, jijini Dar es Salaam.

Samatta ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuendeleza michezo kwa kuwachangia Twiga Star ambapo amesema wanawake wamekuwa wakifanya vizuri, hivyo jamii inawajibu wa kuwasaidia kwa hali na mali ili wafanye vizuri na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa katika michezo.

“Mimi Mbwana Samatta nahodha wa timu ya taifa, natambua kazi kubwa wanayofanya dada zetu wa Twiga Stars katika ramani ya michezo, naungana na serikali yangu nikisema tano kwa Twiga Stars katika tamasha hili la The Orange Concert, ” amesema Samata.

Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Dada Hood inayojishughulisha na kupinga unyanyasaji wa kijinsia wameandaa tmasha la kuichangia Twiga Stars.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dk. Hassan Abbas, amesema siku hiyo imeratibiwa maalum kwa ajili kufanya harambee kuichangia Twiga Stars ikiwa ni mkakati madhubuti ya kuendeleza michezo kwa wanawake hapa nchini.

“Sisi kama wizara yenye dhamana na michezo katika siku ya wanawake nchini tumekuja na kitu cha tofauti, tunaipongeza Twiga Stars, lakini tuna hamasisha wadau na wapenda michezo wote nchini kuichangia ili tuinue michezo kwa wanawake wa hapa,” amesema.

RC Makalla ateta na kamati ya ushauri ya mkoa
Pablo: Simba SC ina nafasi ya kutwaa ubingwa