Rais wa Marekani Joe Biden jana siku ya Jumanne Machi 8, alithibitisha kuwa nchi yake imepiga marufuku ununuzi wa gesi, mafuta, na makaa ya mawe kutoka Urusi.

Rais Biden ametangaza marufuku hiyo ya kuagiza bidhaa za mafuta na nishati kutoka Urusi kama njia mojawapo ya kuiadhibu nchi hiyo kwa kuivamamia kivita taifa la Ukraine.

“Tunapiga marufuku uagizaji wa bidhaa zote za mafuta na gesi kutoka Urusi. Hatua hiyo inamaanisha kuwa bidhaa zote za nishati hatikubaliwa kusafirishwa katika bandari ya Marekani,” Biden aliwaambia wanahabari kwenye Ikulu ya White House.

Wakati hayo yakijiri taifa la Uingereza limesema kwamba litapiga marufuku ununuzi wa mafuta hayo pamoja na bidhaa nyinginezo za nishati mwishoni mwa mwaka huu, ila kuwaruhusu wafanyabiashara na wasambazaji wa bidhaa hiyo muda wa kutafuta njia mbadala.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, nchi yake inapinga vikwazo vya kutoagiza bidhaa za nishati kutoka Urusi.

Baerbock alisema iwapo Ujerumani itazuia kuingia nchini humo kwa bidhaa hizo kutoka Urusi kiasi cha umeme kukatika nchini Ujerumani, watalazimika kuviondoa vikwazo hivyo wao wenyewe, ili uchumi wa nchi usisambaratike.

Hivi sasa Ujerumani inategemea asilimia 55 ya gesi na asilimia 42 ya mafuta na makaa ya mawe kutoka Urusi. Urusi ni muuzaji mkubwa wa mafuta na gesi duniani kote.

Kapombe: Nina imani nitaikabili RS Berkane
Simba SC yampa pole Hassan Dalali