Mamlaka nchini Ukraine zinasema ndege za Urusi zimezishambulia hospitali tatu usiku wa kuamkia Alkhamis (Machi 10) magharibi mwa mji mkuu, Kyiv, na kwenye mji wa bandari wa Mariupol, huku juhudi za uokozi zikiendelea.

Mashambulizi hayo yamekuja kukiwa na matumaini ya kuwahamisha raia kutoka miji kadhaa iliyozingirwa, ukiwemo Mariupol, ambao hauna chakula, maji, wala umeme kwa siku kadhaa sasa.

Mji huo umezingirwa na majeshi ya Urusi kwa siku tisa sasa, huku maafisa wa mji wakisema kuwa wakaazi wake 1,200 wameshauawa na wafanyakazi wa kujitolea wameanza kuzizika maiti kwenye makaburi ya pamoja kutokana na kujaa kwa maeneo ya kuzikia.

Mkuu wa mkoa wa Kyiv, Oleksiy Kuleba, alisema kupitia televisheni kwamba “jeshi la Urusi limeyageuza maisha kuwa jahanamu, ambapo watu wanajificha chini ya mahandaki mchana na usiku wakiwa hawana chakula, maji wala umeme.”

Mji mwengine ulioshambuliwa vikali kwa mabomu ni Zhytomyr wenye wakaazi 260,000 na ulio magharibi mwa mji mkuu, Kyiv. Meya wa mji huo, Serhii Sukholym, alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba “hospitali mbili zilmeshambuliwa, mojawapo ikiwa ya watoto.” 

Katika mji wa pili kwa ukubwa, Kharkiv, makombora ya Urusi yaliharibu makao makuu ya polisi, na kuwauwa watu wanne na kuwajeruhi wengine 15, kwa mujibu wa mwakilishi wa ofisi ya mwendesha mashitaka, Serhii Bolvinov, ambaye aliongeza kuwa tangu uvamizi kuanza wiki mbili zilizopita, wakaazi 282 wa mji huo wameshauawa, sita kati yao wakiwa watoto wadogo.

Hata hivyo kwenye hotuba yake ya kila siku, Rais Volodymr Zelenskyy amesema juhudi zinaendelea kuwaokowa watu 18,000 waliokwama kwenye mkoa wa Kyiv, akiongeza kuwa kufikia Jumatano jioni, watu 35,000 walishakimbilia maeneo salama kupitia njia zilizowekwa kuwaokowa.

chanzo @dw swahili

RS Berkane yaanza safari ya Dar es salaam
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 10, 2022