Mfugaji NarudashwaTitika mwenye umri wa miaka 45 mkazi wa kijiji cha Alaitore kilichopo ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya tembo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi MKoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema kuwa tukio limetokea Machi 9, 2022 majira ya saa saba mchana.

ACP Masejo amesema Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa marehemu alikutwa na mkasa huo wakati akitafuta kuni akiwa na wenzake ndani ya hifadhi  ndipo alipo shambuliwa na tembo huyo, mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi baada ya uchunguzi wa daktari.


Katika tukio jingine Machi 9, 2022 majira ya saa nne asubuhi katika kitongoji cha Karafia kijiji cha Kisimiri Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha askari wakiwa katika operesheni walifanikiwa kuharibu shamba lenye ukubwa wa ekari tano (05) likiwa na miche idhaniwayo kuwa madawa ya kulevya aina ya bhangi.


ACP Masejo amesema kuwa mtuhumiwa wa shamba hilo aliyefahamika kwa jina moja la Babu alitumia mbinu ya kuchanganya miche hiyo ya bhangi pamoja na mazao aina ya mahindi, ambapo juhudi za Jeshi la Polisi mkoani Arusha linaendelea  kumtafuta mmiliki wa shamba hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


Sambamba na hayo yote Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi wanaoishi katika hifadhi kuchukua tahadhari katika maeneo ya hifadhi za wanyama pori na kuhakikisha wanafuata maelekezo mbalimbali  yanayotolewa na mamlaka za uhifadhi, lakini pia ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi hususani kwa kuwatumia askari kata kuhusiana na baadhi ya watu wanao jihusisha na kilimo cha madawa ya kulevya pamoja na uuzwaji wa madawa hayo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Luka Modric amuita Mbappe Real Madrid
Habari Picha:Rais Mwinyi akutana na balozi wa Uholanzi nchini