Serikali ya Kenya sasa inatarajia kulegeza masharti ya afya yaliyowekwa kufuatia mlipuko wa janga la UVIKO-19 miaka miwili iliyopita ikiwemo uvaaji wa Barakoa.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema hayo kwenye mahojiano na kituo cha Citizen TV, Machi 9, kwamba ataondoa sheria ya ulazima ya kuvaa barakoa kufuatia kupungua kwa makali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Kagwe ameeleza kuwa licha ya kupuuzwa kwa wazi kwa sheria hizo, rekodi ziko chini kuashiria kuwa raia wana kinga thabiti na Wizara yake bado inaendelea na utafiti wake na inatarajiwa kutoa tangazo kuhusu kusahisishwa kwa sheria hizo siku chache zijazo.

“Mara ya kwanza nilipogundua hawa watu siku hizi hawajavaa barakoa basi unajiuliza nini kinafuata?, tuangalie tuone. Labda tunaendelea kuwa na kinga yenye nguvu polepole na tunapoendeleza kinga hiyo, hauwi mkali kwao. Hautumii polisi kuwapiga kwa sababu hawajavaa maski,” alisema Kagwe.

Pia aliongezea akisema kuwa, “Ikiwa hawaugui, basi labda huo ndio mwelekeo tunaopaswa kwenda. Huu ni uamuzi ambao tutafanya katika siku chache zijazo.”

Waziri huyo pia alieleza kuwa baadhi ya utafiti unaofanywa ni kuhakikisha kwamba kiwango chanya cha maambukizi kiko chini kwa muda fulani na kwamba hospitali zina vifaa vya kutosha iwapo kutakuwa mlipuko wa homa hiyo tena.

Haya yanajiri huku Kenya ikirekodi kiwango chanya cha asilimia 0.3 mnamo Jumatano, Machi 9, baada ya watu 14 kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona kutoka kwa sampuli 5,585 zilizopimwa.

Rekodi za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa ni watu 27 tu ndio wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) huku 204 bado wako chini ya uangalizi wa nyumbani.

Aliyepandikizwa moyo wa nguruwe afariki dunia
Waratibu tiba asili wapewa jukumu na serikali