Waratibu wa tiba Asili/Mbadala wa Halmashauri wametakiwa kuwaelimisha waganga wa tiba Asili/Mbadala juu ya sheria, miiko na maadili pamoja na usafi wakati wa utoaji wa huduma.

Hayo yamesemwa leo machi 10, 2022 na Mkurugenzi wa tiba Dkt. Omari Ubuguyu wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa tiba Asili/Mbadala jijini Dodoma.

Matumizi ya huduma za tiba Asili/Mbadala yameongezeka na zaidi ya asilimia 60 wanatumia huduma za tiba asili kabla ya kwenda kwenye huduma za kisasa.

Dkt. Ubuguyu ameendelea kutoa wito kwa Waratibu hao kuendelea kuratibu huduma hizo katika Halmashauri zao ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo viovu ambavyo ni kinyume na Sheria ya tiba Asili/Mbadala Na. 23 ya mwaka 2002 ikiwa ni pamoja na kupiga ramli chonganishi.

“Kwa pamoja tuliona muitikio wa jamii juu ya matumizi ya dawa za tiba asili katika kupambana dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, huu ni uthibitisho tosha kuwa huduma hizi zinakubalika na kuaminika na jamii”. Amesema Dkt. Ubuguyu

Amewakumbusha kuwa jukumu la waratibu ni kuhakikisha jamii inapokea huduma salama ambayo haihatarishi Afya ya jamii na hayo yote yatawezekana kama watasimamia shughuli za tiba Asili/Mbadala kwa weledi na nidhamu.

Kwa upande wake Mratibu wa tiba Asili/Mbadala kutoka Morogoro Bi. Elizabeth Kibela ameshukuru wizara ya Afya kupitia Tiba Asili/Mbadala kwa kuanzisha mafunzo hayo.

“Mafunzo haya yataenda kutujengea uwezo mzuri kwa kwenda kuwafundisha wanganga na kuwakumbusha juu ya kufuata sheria, miiko na maadili ya tiba asili”. Amesema Bw. Kibela

Mafunzo hayo kwa waratibu wa tiba Asili/Mbadala yakayo fanyika kwa siku mbili yamehusisha Mikoa minne ambayo ni pamoja na Dodoma, Morogoro, Singida na Tabora.

Kenya kuachana na uvaaji wa barakoa
Uwekezaji washamiri kati ya Tanzania na Saudi Arabia