Sekta ya madini nchini imeweka historia ya mauzo ya moja kwa moja ya madini yenye thamani ya shilingi Trilioni 8.3 kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kuelezea mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita jijini Dodoma leo, Machi 10, 2022, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka robo moja ya mwaka hadi nyingine katika kipindi cha Januari hadi Septemba.

Amesema pia ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za madini umekuwa kutoka asilimia 48 hadi kufikia 63 na kuongeza thamani ya huduma migodini kufikia Dola za Marekani milioni 579.3  sawa na Trilioni 1.33 kutokana na huduma hizo.

Dkt. Biteko amefafanua kuwa mwaka 2021 wastani wa mchango wa sekta hiyo umekuwa hadi kufikia asilimia 7.3 ya pato la Taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi cha mwaka 2020.

Amesema katika robo ya tatu ya Julai hadi Septemba  mwaka 2021, mchango wa sekta hiyo umeongezeka  hadi kufikia asilimia 7.9 ya pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 ya pato hilo katika kipindi kama hicho cha mwaka 2020.


” Matokeo yanaakisi dhamira ya serikali kuhakikisha sekta hii inaimarika  na kuweza kuchangia pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyotangazwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa na Mpango wa Maendeleo, Kwetu sisi sekta ya madini  mwaka huu umekuwa ni mwaka wa kazi na matokeo makubwa ambayo yanaendelea kuleta mageuzi ya kisekta kwa nchi yetu,” amesema Dk. Biteko.

Aidha ameeleza kuwa Wizara hiyo imeongeza usimamizi kwenye madini, ujenzi na viwandani ambapo tayari mifumo ya kielektroni imeanza kutumika katika usimamizi wa mapato ya serikali yatokanayo na madini hayo.


Dk.Biteko amesema katika juhudi za kusimamia  upatikanaji wa mapato kutokana na madini, Wizara imeanza ushirikiano na  Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ili kuweza kuwafikia wananchi watumiaji wa madini waweze kuchangia fedha zitokanazo na shughuli za Uchimbaji madini kwa mujibu wa sheria ya madini.


” Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imeendelea kusimamia na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki kikamilifu  na kwa ufanisi kwenye uzalishaji wa madini hapa nchini, katika usimamizi huu kwa sasa wachimbaji wadogo wanachangia zaidi ya asilimia 30 kwenye mapato yatokanayo  na madini,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko pia ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya 6 imeendelea kushika kasi katika kuongeza ushiriki wa wachimbaji wa wadogo wa madini katika kuongeza pato la Taifa ambapo Jumla ya Leseni 8,172 zimetolewa katika shughuli zote za uchimbaji, utafutaji, uchenjuaji na usafirishaji wa madini ikilinganishwa na Leseni 6, 334 zilizotolewa mwaka 2020 hadi Februari 2021.


Morrison amtumia salamu Ibenge
Wanawake Afrika hatarini zaidi kuugua Ugojwa wa Figo