Meneja wa Habari na Mawasilino wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally, amesema kikosi chao kinaendelea kufanya maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko wanne wa ‘Kundi D’, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa ‘Kundi D’, Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ahmed amesema Kocha Pablo Franco amewataka wachezaji wa Simba SC kuwa makini kwenye mchezo huo, ambao wanapaswa kusaka matokeo ya ushindi, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

“Silaha zetu ziko kambini na wachezaji wana molari, hali ya kujiamini na kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo huo kwa kuibuka na ushindi mkubwa na kuongoza kundi letu ni ya kiwango cha juu,” amesema Ahmed Ally

Ameongeza kwa kuwataka RS Berkane wajipange kutokana na aina ya maandalizi waliyofanya lakini pia kurejea kwa wachezaji wao waliokuwa majeruhi kumekifanya kikosi chao kukamilika na kuwa tayari kwa mapambano.

“Wachezaji wako fiti zaidi kuhakikisha tunafikia malengo ya kushinda mchezo huu wa nyumbani, tumejipanga kuzibakisha alama tatu hapa hapa, tunaamini hilo litatimia, tuko tayari kwa vita.” amesema Ahmed Ally

Simba SC ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Kundi D, Februari 27 mjini Berkane-Morocco hivyo itahitaji kulipa kisasi kwa kusaka ushindi ili kurejea kileleni mwa msimamo wa Kundi hilo.

Kabla ya mchezo huo Simba SC ilikua inaongoza msimamo wa Kundi D kwa kuwa na alama 04, huku Berkane iliyopoteza mchezo wa Mzunguuko wa pili dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ilikua na alama 03.

Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.

Mbunge Mafuwe: sina chuki na mbowe
Amos Makalla awaita mashabiki Kwa Mkapa