Mgombea Urais wa Kenya kupitia chama cha Jubilee, William Ruto jana jumapili Machi 13 ametoa ya Moyoni baada ya kumwambia ukweli Rais Uhuru Kenyatta kuwa kumuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga ni kumsaliti yeye.

Ruto alisema kwa miaka minne amekuwa akihangaishwa na serikali ambapo alikuwa anamsaidia Rais Uhuru kuiunda na kuonekana kukerwa huku akimkumbusha Rais Uhuru kazi ambayo walimfanyia 2013 na 2017 hadi akachaguliwa.

“Sisi ndio tulitembea na wewe Kenya mzima, tukakutafutia kura, tukapanga mpaka ukakuwa rais. Tukakupigia kura mara tatu, sisi ambao unatudhulumu, sisi ambao unatupiga vita, sisi ambao unatutusi,” alisema DP Ruto huku akimaliza kuwa wanatangatanga wameamua kuachia Mungu kuwaadhibu wale ambao wamewafanyia mabaya.

DP. Ruto alisema mpango wa mageuzi ya katiba kupitia mswada wa BBI ilikuwa ni njama ya kumsaidia Raila kuchukua mamlaka.

“Mimi nataka nikwambie Mheshimiwa ndugu yangu rais, sisi tunaona yale umetufanyia. Lakini kwa sababu sisi ni watu wa kumcha Mungu, tumekusamehe na kukuachia Mungu, Umetufukuza kwenye makamati ya bunge, umevunja chama chetu cha Jubilee, umetuita majina Tangatanga, umetuita takataka, lakini nataka nikwambie sisi ambao unatuita majina, tulitembea na wewe,” alisema DP Ruto.

Wakati huo huo Rais Uhuru Kenyatta amemsifu Kalonzo Musyoka kwa kukubali kuingia Azimio kwa kumuunga mkono Raila Odinga kuwania urais akimsifu kuwa alionyesha uzalendo mkubwa akitaja hatua yake kama nafasi ya kuiokoa nchi.

“Wengi wameweka kando tamaa ama ambitions zao kwa sababu wanataka kuona Kenya ikishikana, mmoja wao akiwa ndugu yangu Kalonzo Musyoka, ameweka tamaa yake chini kwa kulilia taifa la Kenya…nataka tusimame tumpigie makofi kwa sababu ya ushujaa wake. Tunamshukuru na tunamwambia asante sana,” Rais Uhuru alisema.

Rais amekuwa akifanya juhudi kuhakikisha kuwa Kalonzo anaingia Azimio ili kuongeza nafasi za muungano huo ukishinda uchaguzi wa urais ambapo juhudi zake zilizaa matunda jana baada ya Kalonzo kutangaza kuwa Raila ndiye chaguo lake katika kurithi mamlaka Agosti.

Kalonzo anaaminika kuongeza nguvu muungano wa Azimio katika kadi yao ya kupambana na naibu rais William Ruto wakati wadadisi wakisema uwezekano ni atakuwa mgombea mwenza wa Raila.

Hata hivyo, hilo linasemekana huenda likazua joto la kisiasa kutoka kwa wanasiasa wa Mlima Kenya ambao pia wanamezea mate wadhifa huo.

Waziri Mchengerwa: TFF ongezeni viwanja kituo cha michezo Tanga
Sanga amvaa Rage, Hii sio ligi ya Mbuzi