Uongozi wa Young Africans umesema upo tayari kumuuza mchezaji yoyote mwishoni mwa msimu huu, endapo itapata ofa nzuri inayoendana na thamani ya mchezaji husika.
Young Africans imetoa taarifa hizo, kufuatia tetesi zilizochukua nafasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii Juma Lililopita zilizomuhusu Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele.
Imedaiwa kuwa Mshambuliaji huyo anawindwa na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kufuatia uwezo wake mkubwa tangu alipojiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS Vita Club ya nchini kwao DR Congo.
Mwenyekiti wa kamati ya Usajili ya Young Africans, Engneer Hersi Said amesema hakuna mchezaji atakayezibiwa riziki kama atatakiwa na klabu ya ndani au nje ya Tanzania, ilimradi taratibu zifuatwe.
“Hatuwezi kuwabania wachezaji hata kidogo. Yeyote atakayepata nafasi ya kutoka tutamuachia atoke akajaribu maisha kwingine.”
“Mpira siku hizi ni zaidi ya ajira, Tulimuuza Kisinda kwa kuvuna dola 150,000 kupitia mauzo ya mchezaji mmoja tuliwanunua mastaa watatu Djuma Shabani, Fiston Mayele, na Jesus Moloko wote wanafanya vizuri” amesema Hersi Said
Mayele ndio anaongoza katika upachikaji mabao kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22 akifunga mabao 10, sawa na Mshambuliaji wa Namungo FC Reliant Lusajo.