Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema hawana shaka na kikosi chao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.

Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ kwa kufikisha alama 07, baada ya kuibanjua RS Berkane bao 1-0 Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Try Again amesema Uongozi wa Simba SC umekua ukifanya kazi zake kwa umakini mkubwa ili kutimiza lengo la kikosi chao kupata ushindi, na hilo limekua likitokea, hivyo wachezaji wanajua majukumu yao.

Amesema kwa mfumo huo, anaamini Simba SC itafika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku akikumbushia mipago yao ni kufika Nusu Fainali na ikiwezekana kutinga Fainali na Kutwaa Ubingwa.

“Benchi la ufundi limefanya kazi ya kutosha kuandaa timu kimbinu na kiufundi zaidi, wachezaji wamekwenda kupambana vya kutosha na kuhakikisha tunashinda na imekuwa hivyo,” amesema Try Again

“Hatuna wasiwasi ushirikiano unaotoka kwetu uongozi kwenda kwa wachezaji na benchi la ufundi Simba, tunaamini tutafanya vizuri zaidi katika mashindano haya na kufika hatua za mbele tofauti na misimu mingine yote katika mashindano.” ameongeza kiongozi huyo

Simba SC inajiandaa na mchezo wa Mzunguuko watano wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast utakaopigwa nchini Benin Jumapili (Machi 20).

Mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Simba SC ilichomoza na ushindi wa mabao 3-1.

Wakati Simba SC ikitakapokua ugenini nchini Benin, mchezo mwingine wa Kundi D, utapigwa mjini Niamey-Niger kati ya USGN itakayokua mwenyeji wa RS Berkane kutoka Morocco.

TBS yatoa semina kwa wadau sekta ya dawa na vifaa tiba
Tanzania kusikika mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani