Katika kuelekea Siku ya Viwango Barani Afrika yatakayofanyika Machi 31,2022 mkoani Arusha, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa Semina ya wadau katika Sekta ya Dawa na Vifaa Tiba ambayo imefanyika leo Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akifungua Semina hiyo Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt.Athuman Ngenya amewaasa wadau wa sekta ya dawa na vifaa tiba waliohudhuria semina kutumia fursa ili kujifunza na kueleza changamoto za viwango zilizopo katika sekta hiyo ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Amesema kuwa Viwango ni nyaraka ambazo hutayarishwa kwa kuzingatia mfumo wa uwazi na ushirikishaji wa wadau mbalimbali na vinapokuwa vimekamilishwa na kupitishwa na mamlaka husika, viwango huweka maanisho na misingi muhimu ya kuzingatia katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, utoaji huduma katika maeneo mbalimbali ya jamii na utendaji katika sekta mbalimbali ikiwemo madawa na vifaa tiba.
Aidha Dkt.Ngenya amesema Matakwa ya viwango yanazingatia kuwezesha kutolewa kwa bidhaa na huduma bora kwa jamii husika hivyo kulinda afya, usalama na mazingira na hatimae kuchangia katika uchumi endelevu wa taifa.
“Viwango hivi pia huainisha matakwa ya msingi ya bidhaa au huduma ambayo humwezesha mtumiaji wa kiwango hicho kuweka taratibu au kanuni zitakazomuwezesha kudhibiti utendaji kazi wake na kutoa bidhaa au huduma bora kwa wakati wote”. Amesema Dkt.Ngenya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango (TBS) Mhandisi Yona Afrika amesema lengo la kuandaliwa kwa semina ya wadau wa dawa ni kujadili Jukumu la Viwango katika kukuza sekta ya dawa na vifaa tiba Afrika, kufikia kujitegemea na ustahimilivu katika kupambana na UVIKO-19 na magonjwa mengine ya mlipuko.