Wawakilishi wa Tanzania kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Simba SC, kesho Ijumaa (Machi 18) wataanza safari ya kuelekea Benin tayari kwa mchezo wa Mzunguuko watano wa ‘Kundi D’.
Simba SC inatarajiwa kuondoka Dar es salaam alfajiri kuelekea Benin ambako Jumapili (Machi 20) itapapatuana na ASEC Mimosas ya Ivory Coast katika Uwanja wa de l’Amitié, mjini Cotonou-Benin.
Taarifa ya Simba iliyotolewa mapema leo Alhamis (Machi 17), imebainisha kuwa kikosi kitaondoka saa Tisa Alfajiri kikiwa na Wachezaji 24, Benchi la Ufundi na baadhi ya Viongozi.
Simba SC inakwenda ugenini ikiwa inachagizwa na matokeo ya bao 1-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco, ushindi iliyoiwezesha kuongoza msimamo wa Kundi D kwa kufikisha alama 07.
Nafasi ya pili katika kundi hilo inashikwa na ASEC Mimosas yenye alama 06 sawa na RS Berakane, huku Union Sportive Gendarmerie Nationale ‘USGN’ ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 04.
Wakati Simba SC ikicheza dhidi ya ASEC Mimosa ugenini siku ya Jumapili (Machi 20), RS Berkane itakua mgeni wa Union Sportive Gendarmerie Nationale ‘USGN’ mjini Niamey katika Uwanja wa Général Seyni Kountché.