Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya KMC FC Christina Mwagala, amesema kikosi chao kina uwezo wa kuifunga Young Africans kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 18 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Miamba hiyo ya Dar es salaam itakutana kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa kusaka alama tatu muhimu za Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia mishale ya saa moja jioni.
Christina amesema wanatambua Young Africans ina kikosi bora msimu huu, na wanakipa heshima kama ilivyo kawaida yao, lakini kwa maandalizi waliyoyafanya kuelekea mchezo huo, wanaamini mambo yatawanyookea na kuwa timu ya kwanza kuifunga miamba hiyo ya Jangwani msimu huu 2021/22.
“Pamoja na ubora waliyonao Young Africans bado ni timu ambayo inafungika, sasa basi sisi ndo wenye password ya kuifunga Young Africans, tunakwenda kuwa timu ya kwanza kuifunga.” amesema Christina
Mchezo wa Duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo mjini Songea Mkoani Ruvuma katika Uwanja wa Majimaji, Young Africans ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa 2-0, mabao yakifungwa na Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 45 iliyozivuna katika michezo 17 waliyocheza hadi sasa, huku KMC FC ikishika nafasi ya 07 ikiwa na alama 22.