Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania, TMDA imepiga marufuku kutumia bidhaa za tumbaku katika maeneo yasiyo rasmi ili kuilinda jamii kiafya
Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Kati Sonia Mkumbwa, akizungumza kwenye kikao kazi cha kutoa uelewa wa Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, amesema ni vizuri kwa watumiaji wa bidhaa za tumbaku kutengewa maeneo maalumu ya matumizi ya bidhaa hizo ili kuzuia matumizi ya hadharani ambayo huathiri wengine ambao hawatumii tumbaku.
“Ni vizuri sasa watumiaji wa bidhaa za tumbaku (wavutaji wa sigara) kutengewa maeneneo maalumu ya kutumia bidhaa hizo ambazo zitawekwa vibao vikavyoyaonesha maeneo hayo ili iwe rahisi kutambulika badala ya hivi sasa ambapo matumizi yake yamekuwa yakifanyika hadharani, ” amesema Mkumbwa.
Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Lanslaus Choaji, Mkoa wa Singida, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati akifungua kikao kazi hicho alisema mafunzo hayo yana lengo la kupeana uelewa wa shughuli za udhibiti wa matumizi ya bidhaa za tumbaku katika mkoa wa Singida Pamoja na utekelezaji wake unaofanyika nchi nzima.
“Nafahamu kuwa TMDA imekasimishwa jukumu hili la udhibiti wa matumizi ya bidhaa za tumbaku na Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya Afya Aprili 30, 2021. Hivyo basi, nawapongeza sana kwa kulipokea jukumu hili na bila kuchelewa mmeweza kuandaa mpango kazi wa miaka mitatu 2021/2022 hadi 2023/2024) wa utekelezaji wa shughuli za udhibiti wa bidhaa hizi lengo likiwa ni kupunguza ama kuzuia matumizi ya bidhaa za tumbaku na madhara makubwa ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa hizi,” amesema Choaji.
Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha matumizi ya bidhaa za tumbaku yamekuwa yakiongezeka kwa kasi ulimwenguni ambapo chimbuko lake ni nchi zilizoendelea lakini kwa sasa imebanika kuwa matumizi makubwa ya bidhaa hizo yako katika nchi zinazoendelea.
“Takwimu zimebainisha kuwa zaidi ya watu bilioni 1.3 ya watumiaji wa bidhaa za tumbaku duniani wako katika nchini zetu zinazoendelea. Aidha, tafiti hizo zimebainisha madhara makubwa yaliyoelezwa ni pamoja na vifo vya zaidi ya watu milioni 7 duniani kila mwaka vinavyosababishwa na magonjwa yanayotokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.
Kikao kazi hicho cha kutoa uelewa wa Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku kilimewakutanisha TMDA, Uongozi wa Wafanyabiashara na Viongozi wa ngazi ya mkoa na Manispaa ya Singida.