Rais Vladimir Putin wa Urusu alijitokeza hadharani katika sherehe za kumbukumbu ya miaka nane tangu Urusi ilipoitwaa rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014, Putin alitumia sherehe hizo kusifu vikosi vyake vinavyopigana huko Ukraine “Bega kwa bega, wanasaidiana,” alisema Putin akiongeza kwamba nchi haijawahi kuwa na umoja kama huo kwa muda mrefu.

Putin pia amefanya mazungumzo na kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambapo amesema kwamba Moscow inafanya kila linalowezekana kuepusha madhara kwa raia.

Rais Macron ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya mji wa Mariupol ulioko mashariki mwa Ukraine ambao umezingirwa na vikosi vya Urusi, na kutoa wito wa kusitisha mapigano.

Wakati huohuo vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi katika miji ya Ukraine ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kyiv, na kukishambulia kituo cha ukarabati wa ndege nje kidogo ya mji wa Lviv, karibu na mpaka wa Poland.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House Jen Psaki amesema rais Biden ameelezea jitihada za Marekani na washirika wake katika kushughulikia uvamizi wa Urusi, ikiwemo kuiwekea vikwazo vikali Moscow. Aidha Biden amesisitiza utatuzi wa kidiplomasia katika mgogoro huo.

Nayo Wizara ya mambo ya nje ya China imesema kuwa rais Xi amemwambia Biden kwamba vita nchini Ukraine ni lazima ikomeshwa haraka iwezekanavyo na kutoa wito kwa jumuiya ya kujihami NATO kufanya mazungumzo na Moscow. Hata hivyo kiongozi huyo hajashutumu uvamizi huo wa Urusi kwa mujibu wa taarifa ya Beijing.

Maelfu wafurika kumpokea Mbowe KIA
Mwakalebela: Young Africans tishio barani Afrika