Makamu Mwenyekiti wa Young Africans Fredrick Lameck Wilfred Lugano Mwakalebela ameibuka na kudai kikosi chao kina ubora wa kutisha katika ukanda wa Bara la Afrika msimu huu 2021/22.
Mwakalebela ambaye alikua kimya kwa muda mrefu amesema Kikosi chao kwa sasa kimekua na mwendelezo wa kipekee katika ligi za ndani za Afrika, jambo ambalo linaufariji Uongozi wao ambao ulipambana kukitengeneza.
Amesema katika ligi za ndani za nchi ya Afrika, Young Africans imekuwa sehemu ya klabu ambazo hazijapoteza mchezo wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22, kutokana ubora na umakini waliojiwekea kwa timu yao na kwa mchezaji mmoja mmoja.
“Sio siri kwa sasa Young Africans ni timu tishio Afrika, mpaka sasa nimefatilia Ligi za nchi zote Afrika msimu huu Young Africans ndio timu pekee Haijafungwa na sasa wapinzani wanajua wakija Kukutana na sisi hawatoki, na moto utaendelea hadi tubebe ubingwa wa Ligi Kuu.” amesema Mwakalebela.
Young Africans baadae leo Jumamosi (Machi 19) itacheza mchezo wa Mzunguuko wa 18 wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 45, huku KMC FC ikiwa nafasi ya 07 kwa kufikisha alama 22.