Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Barbara Gonzalez, amesema Uongozi wa klabu hiyo hauwezi kumlaumu yoyote kufuatia matokeo ya kupoteza mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas jana Jumapili (Machi 20).

Simba SC ilikuwa mgeni wa ASEC Mimosas katika mchezo huo wa Kundi D, uliopigwa mjini Cotonou -Benin, ambapo wawakilishi hao wa Tanzania walikubali kichapo cha mabao 3-0.

Barbara amesema kuwa, sio wakati wa kulaumiana sasa wala kunyoosheana vidole kwa matokeo hayo bali ni kujipanga kwa ajili ya mchezo wa mwisho dhidi ya US Gendarmerie ya Niger.

“Tunatakiwa tujipange kwa ajili ya mchezo wa mwisho, kwani bado tuna nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali kama tutashinda na US kwa hiyo hatupaswi kupoteza lengo,” amesema Barbara.

Katika harakati za kufikia lengo Mtendaji huyo amesema, baada ya kurejea kesho Jumanne (Machi 22), wachezaji wote Machi 27 watatakiwa kurejea mazoezi na kuanza kambi ya kuelekea mchezo huo.

Katika Msimamo wa ‘Kundi D’ Simba SC imeporomoka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu ikiwa na alama 07 sawa na RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya pili, huku ASEC Mimosas ikiongoza kwa kufikisha alama 09.

USGN inaendelea kuburuza mkia wa kundi hilo kwa kufikisha alama 05, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya RS Berkane jana Jumapili (Machi 20), ikiwa nyumbani Niger.

Michezo ya mwisho ya ‘Kundi D’ itachezwa April 03, ambapo Simba SC itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kucheza dhidi ya USGN, huku ASEC Mimosas ikisafiri kulekea mjini Berkane-Morocco kupambana na wenyeji RS Berkane.

Mshindi wa kwanza na wapili katika kundi hilo watatinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.

Tanzania, EU zakutana kujadili EPA
Faru Rajabu aaga dunia