Meneja wa klabu ya Juventus FC ya Italia Massimiliano Allegri amesema hana uhakika kama Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Argentina Paulo Exequiel Dybala atabaki klabuni hapo.
Dybala anatajwa kuwa kwenye mpango wa kuondoka Juventus FC mwishoni mwa msimu huu kwa kisingizio cha kutaka changamoto mpya baada ya kuitumikia klabu hiyo tangu mwaka 2015.
Allegri aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo wa Ligi ya Italia dhidi ya Salernitana kuwa, haamini kama Dybala atabakia klabuni hapo, licha ya kucheka na nyavu kwenye ushindi wa mabao 2-1.
“Sifahamu kama ataendelea kuwa mchezaji wa Juventus au la! Ndiyo maana tuna klabu na mimi nipo katika mstari huo. Si Paulo (Dybala) pekee mkataba wake unakaribia kuisha, pia kuna Juan Cuadrado, Federico Bernardeschi na De Sciglio,” alisema Allegri.
“Kwa upande wangu, na kwa upande wa timu, kuna suala la nia ya kufanya vizuri pekee. Ninafanya tathmini ya wachezaji, lakini kuna masuala mengi ikiwa ni pamoja na mikataba.” amesema Allegri
Klabu ya Liverpool ya England inahusishwa na mpango wa kutaka kumsajili Paulo Dybala.