Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Edo Kumwembe ameitahadharisha Simba SC kuwa makini na mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho dhidi ya USGN ya Niger.
Simba SC itakua mwenyeji wa USGN April 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho.
Edo amesema Simba SC inapaswa kuwa makini katika mchezo huo, kutokana na wapinzani wao USGN kuwa na sifa ya kuwa na kikosi bora chenye uwezo wa kufunga mabao kupitia kwa Mshambuliaji na Nahodha wao Victorien Adebayor Zakari Adje.
Edo Kumwembe amesema: “USGN wanaonekana kuwa bora katika ufungaji hasa kupitia kwa mshambuliaji wao anayeitwa Adebayor. Inawezekana yeye ndiye ambaye anaweza kuamua matokeo ya mchezo Uwanja wa Mkapa.”
“Akibanwa vyema basi Simba SC itapita, asipobanwa vyema tunaweza kuwa na MSIBA mwingine kama ilivyotokea katika mchezo dhidi ya UD Songo au Jwaneng Galaxy ya Botswana.”
“Mara nyingi tuna kumbukumbu nyingi nzuri za Simba dhidi ya wakubwa kama Al Ahly, AS Vita, JS Saoura na wengineo katika Uwanja wa Mkapa.”
“Hata hivyo, huwa tunaamua kusahau kumbukumbu hizi mbaya ambazo zaidi zilikuwa mechi za kufa na kupona kwa Simba. Tuchague kumbukumbu hizi mbaya kwa ajili ya kuwakumbusha Simba kazi ambayo inawakabili mbele yao.”
“Hawa wote wawili walionekana kuwa vibonde kwa Simba na kama vile wangekufa nyingi Uwanja wa Mkapa, lakini hadithi ikawa tofauti.”
Simba SC yenye alama 07 kwenye msimamo wa ‘Kundi D’ itahitaji ushindi katika mchezo huo ili ifikishe alama 10 ambazo zitaiwezesha kushika nafasi ya kwanza ama ya pili, huku ASEC Mimosas na RS Berkane nazo zitakua zikiwania nafasi hizo kupitia mchezo wa mwisho utakaozikutanisha mjini Berkane nchini Morocco.
Kwa sasa Msimamo wa ‘Kundi D’ ASEC Mimosas inaongoza kwa kufikisha alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane yenye alama 07 sawa na Simba SC, huku USGN ikiburuza mkia kwa kumiliki alama 05.