Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Kassim Dewji amesema Uongozi wa klabu hiyo utafikia makubaliano na baadhi ya wachezaji wanaomaliza mikataba yao, baada ya kupokea ripoti ya Kocha Mkuu Franco Pablo Martin.
Baadhi ya wachezaji wa Simba SC wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu ni viungo Bernard Morrison, Hassan Dilunga, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, na Said Ndemla anayecheza Mtibwa Sugar kwa mkopo, mabeki Pascal Wawa, Joash Onyango na Ame Ibrahim anayekipiga pia Mtibwa kwa mkopo.
Wengine ni kipa Aishi Manula na washambuliaji Meddie Kagere na Chris Mugalu.
Awali ilielezwa Onyango alishafanya mazungumzo na mabosi wa Simba, lakini akaweka masharti yake ikiwamo kuongezewa mshahara na masilahi mengine na kuwafanya mabosi hao kurudi nyuma wakielekeza nguvu kwenye mechi za hatua ya makundi ya Shirikisho.
Kassim amesema Kocha Pablo ndiye mwenye maamuzi ya mwisho ya kusema anahitaji kufanya kazi na mchezaji wa aina gani, hivyo bado ni mapema sana kusema nani na nani watasaini mikataba mpya ndani ya klabu hiyo inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikishio Barani Afrika.
“Kocha ndiye mwenye kutuletea maamuzi juu ya wachezaji wake tunafanya utekelezaji tu, akisema mchezaji huyu simuhitaji hatuweza kubisha tunatafuta anayemuhitaji ili kuboresha kikosi zaidi na hiyo ndiyo kazi yetu kama kamati.”
“Sasa hivi akili zetu zipo sana kwenye michuano hii muhimu ambapo nchi yote inatuangalia sisi, na kama mabingwa watetezi wa ligi na FA tunatakiwa kupambana zaidi, tukishamaliza haya mashindano naweza kuwa huru sasa kujikita katika usajili,” amesema Dewji ambaye ni mkongwe ndani ya uongozi wa Simba.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema watafanya usajili wa kishindo kwa kuongeza nyota wanne wa kimataifa.
Inafahamika kuwa tayari Simba SC imeshamalizana na nyota kutoka Zambia, Moses Phiri atakayejiunga na Wekundu hao Agosti, mwaka huu na mikakati ya kumnasa Adebayor wa USGN iko pazuri.