Kocha Mbwana Makata amesema ana kazi kubwa ya kufanya baada ya kukubali kufanya kazi na klabu ya Mbeya Kwanza FC ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

Kocha Makata alitangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza FC mwanzoni kwa juma hili, akichukua nafasi ya Mwaka Mwalwisi aliyerejea kwenye nafasi yake ya Ukurugenzi wa ufundi klabuni hapo.

Kocha huyo aliyekua anakinoa kikosi cha Dodoma Jiji FC, amesema baada ya kuanza kazi ameona kuna mambo mengi ya kuyaboresha kwenye kikosi chake, ili kufanikisha azma ya kuibakisha Mbeya Kwanza FC kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao wa 2022/23.

“Kazi yangu kubwa hapa ni kuhakikisha Mbeya Kwanza FC haishuki daraja, na kila mmoja anaona timu haipo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo, hivyo nitapambana ili kuibakisha Ligi Kuu.”

“Kazi ya kwanza niliyonayo hapa ni kujenga upya Saikolojia ya wachezaji, na nyingine ni kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza siku za nyuma ili kuondoa makosa ambayo yameifikisha timu hapa ilipo.”

“Pia nitaendeleza mazuri yaliyofanywa na watungulizi wangu katika klabu hii, ninaamini hakuna linaloshindikana, Uongozi umenihakikishia kunipa ushirikiano wa kutosha ili tufanikishe lengo la kuiona Mbeya Kwanza FC ikiendelea kucheza Ligi Kuu msimu ujao.” amesema Kocha Mbwana Makata

Mbeya kwanza FC ipo nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imejikusanyia alama 14, zilizotokana na ushindi wa michezo 02, sare katika michezo 08 huku ikipoteza michezo 08.

Kocha Dodoma jiji aihofia Tanzania Prisons
Twaha Kiduku: Nipo tayari, Sitawaangusha