Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC Masoud Djuma Irambona amesema mchezo unaofuata dhidi ya Tanzania Prisons hautakua rahisi kwake na kwa wachezaji wake, kutokana na ubora wa kikosi cha maafande hao wa Jeshi la Magereza.
Dodoma Jiji FC itasafiri hadi jijini Mbeya kuikabili Tanzania Prisons April 02 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokione, Mchezo ambao unatabiriwa kuwa na vuta ni kuvute kutokana na Maafande wa Magareza kuhitaji kujiondoa kwenye nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu.
Kocha Masoud ambaye amekabidhiwa jukumu la kuliongoza benchi la ufundi la klabu hiyo, akichukua nafasi ya Kocha Mbwana Makata amesema anaifahamu Tanzania Prisons kuwa ni timu ngumu na yenye mbinu za ajabu katika soka la Bongo, hivyo hana budi kujipanga ili kuikabili ipasavyo.
“Ni timu ngumu sana, tangu nije hapa Tanzania wakati ule niko na Simba SC ni timu ambayo ilikua inatupa wakati mgumu sana, imeendelea kuwa hivyo hadi sasa, sina budi kujiandaa vizuri kimbinu ili kuikabili tutakapocheza nayo kwenye Uwanja wake wa nyumbani.”
“Kweli hii timu mimi siipendi kwa sababu ina uchezaji wa tofauti kabisa, wakati ule nipo Simba walitusumbua sana, sasa kama walisumbua timu kubwa kama Simba SC, sisi itakuwaje?, ndio maana ninasema siipendi.”
“Hata nafasi waliopo kwa sasa nayo itaongeza upinzani mkubwa sana katika huu mchezo tunaokwenda kucheza nao, nina kazi kubwa sana nikishirikiana na wasaidizi wangu, kwa sababu hautokua mchezo rahisi hivyo.” amesema Kocha Masoud Djuma.
Katika Duru la Kwanza Dodoma Jiji FC inayoshika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 21, iliifunga Tanzania Prisons mabao 2-1 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.