Kocha Msaidizi wa Young Africans , Cedrick Kaze ametoa siri za wachezaji wawili ndani ya kikosi hicho (Farid Mussa na Yannick Bangala).
Kaze ambaye ni raia wa Burundi anayetumia muda mwingi mtandaoni kujifunza soka la kisasa, amesema Bangala ni moja ya wachezaji wazoefu akicheza beki wa kati amekuwa na faida kutokana na utulivu pamoja na maamuzi sahihi aliyokuwa nayo.
“Bangala kuna wakati Young Africans tunakuwa tunashambuliwa anaweza kukaba na mara baada ya kupata mpira amekuwa akifanya maamuzi sahihi yanayoiweka timu katika wakati salama,” amesema Kaze.
“Wakati tunashambulia Bangala anaweza kuanzisha mashambulizi na amekuwa mtulivu wa kufanya maamuzi sahihi katika nyakati zote mbili kushambuliwa na kushambulia,”
“Mchezaji kama Bangala amekuwa na faida kubwa katika kikosi chetu kutokana na uzoefu wake kuna muda anawapa maelekezo wenzake uwanjani jambo gani la kufanya kwa kati huo.
“Anaweza kucheza nafasi zaidi ya moja kwenye kiwango bora kile kile na sifa nyingi bora alizokuwa nazo anaweza kuwa nahodha katika timu yetu,”alisema Kaze ambaye amewahi kufanya kazi kwenye akademi ya Barcelona kwa mafanikio.
Akimzungumzia Farid aliyewahi kucheza Hispania, anasema ni moja ya wachezaji wenye akili na uwezo wa kushika mafundisho, maelekezo kwa haraka zaidi anayopatiwa na kocha wake.
“Kutokana na akili hiyo ya kuelewa haraka kile anachofundishwa anaweza kucheza nafasi nyingi zaidi kwa sasa tunamtumia kama beki wa kushoto na amekuwa akifanya vizuri jambo ambalo linakuwa ngumu kumuweka nje mchezaji wa aina yake,” alisema Kaze na kuongeza;
“Ukiangalia msimu huu tumemtumia Farid winga kushoto na kulia, beki wa kushoto, kiungo mshambuliaji na nyuma ya mshambuliaji si rahisi kutumika kwenye maeneo haya yote kama hafanyi vizuri,”
“Farid anatumika beki wa kushoto na wapo wengine watatu katika nafasi hiyo inakuwa ngumu kumuweka nje kwani anaweza kutumiza majukumu ya kukaba mawinga wa timu pinzani pamoja na kushambulia kwani ndio sifa yake ya kwanza.”
Chanzo: Mwanaspoti