Swali lililobaki miongoni mwa wadau na wafuatiliaji wa kiwanda cha muziki Tanzania ni kuwa ni nani ataihodhi nafasi ya kuwa msemaji wa Shirikisho la muziki Tanzania na lini atatajwa, punde baada ya msemaji mteuliwa kujiondoa katika nafasi hiyo.

Kufuatia kupingwa vikali na idadi kubwa ya wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa muziki kwa madai hakustahili kuhudumu katika nafasi hiyo, hii leo Steve Mengele amejiuzulu rasmi nafasi hiyo.

Wakati maelfu ya watu wakiwa katika sintofahamu hiyo, kutoka kundi la Weusi mwanamuziki mahiri George Sixtus Mdemu, maarufu G Nako ameweka wazi mtazamo wake kuhusu mtu sahihi anayestahili kuhudumu kama msemaji wa Shirikisho la Muziki Tanzania na kukidhi hitaji la nafasi hiyo ili kuleta mabadiliko kulingana na matakwa ya katiba inayoliongoza Shirikisho hilo.

“Kwanza hiyo nafasi haikuwepo, ndo imekuja sasa hivi lakini inabidi tupate mtu ambaye ana uelewa na kile anachoenda kukifanya nadhani AY, Wakazi, au Mwana Fa wanaweza kuifanya hiyo kazi vizuri,” alisema G Nako.

G Nako, ameyasema hayo alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalum na kipindi cha XXL, ambapo aliendelea kusisitiza kuwa lazima sanaa ya muziki ipate mtu mwenye maslahi na muziki na wa manufaa ya sasa na baadae.

Ngorongoro yaikutanisha serikali na mabalozi
Cedric Kaze awachambua Farid Mussa, Bangala