Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umekanusha taarifa za kumpa mtihani Kocha Mkuu Franco Pablo Martin wa kuhakikisha anaifunga US Gendamarie ya Niger Jumapili (April 03), na endapo atashindwa utamfuta kazi.

Simba SC imekanusha taarifa hizo, baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilidai kuwa Kocha Pablo amekalia kuti kavu klabuni hapo, huku mchezo dhidi ya US Gendamarie ukitajwa kuwa mtihani wa mwisho kwa kocha huyo kutoka nchini Hispania.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema taarifa hizo ni za kutungwa na zimeanzishwa makusudi na baadhi ya watu wasioitakia mema klabu hiyo, zikiwa na lengo la kupoteza utulivu.

Ahmed amesema kuwa ni kweli walimpa kocha Pablo malengo ya kuifikisha Nusu Fainali, lakini hakuna sehemu yoyote waliyowahi kumwambia kuwa asipowafikisha watamtimua.

“Lengo la taarifa hizo za kutungwa ni kwa ajili ya kupoteza utulivu ndani ya klabu, hasa kuelekea kwenye pambano hilo muhimu. Ni kweli kocha tulimpa malengo ya kuifikisha timu nusu fainali, lakini hatukumwambia tusipofika tutamfukuza,” amesema.

“Ikitokea tukifika tutafurahi kwa sababu tumeweza kufikia malengo, lakini ikitokea tumekwama tutakaa chini na mwalimu tutamuuliza amekwama wapi atatuambia au atatupa sababu zake, na uongozi utakaa na kuzifanyia kazi, baada ya hapo maamuzi ya kimaslahi ya pande mbili yataamualiwa,”

“Lakini kwa sasa bado ni kocha wetu, hana wasiwasi na tunamuamini, ameleta mafanikio makubwa sana kwenye kikosi cha Simba kwa timu nzima na mchezaji mmoja mmoja, kuna sababu gani ya kumuwekea presha?” Amehoji Meneja huyo.

Simba SC itatakiwa kushinda dhidi ya US Gendamarie Jumapili (April 03), ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Robo Fainali Kombe la Shirikisho msimu huu 2021/22.

Simba SC ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi D, ikiwa na alama 07 sawa na RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya pili, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiwa kileleni kwa kuwa na alama 09.

US Gendamarie ya Niger itakayocheza dhidi ya Simba SC Jumapili (April 03) inashika nafasi ya nne kwenye kundi hilo kwa kuwa na alama 05.

Kocha Mafunzo FC aitahadharisha Young Africans
Dkt. Mabula ataka elimu itolewe ugawaji wa ardhi