Kocha Msadizi wa Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Selemani Matola, amesema makosa walioyafanya kwenye mchezo dhidi ya ASEC Mimosas wanayatumia kama sehemu ya maandalizi ya kuelekea mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya US Gendarmerie ya Niger.
Simba SC itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumapili (April 03), huku ikihitaji kushinda dhidi ya US Gendarmerie, ili kujihakikishia nafasi ya Kucheza Hatua ya Robo Fainali.
Matola amesema wameona mapungufu kupitia mchezo dhidi ya ASEC Mimosas, hivyo baada ya kuingia kambini, wameanza kuyafanyia kazi kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya US Gendarmerie.
Ameongeza kuwa, kati ya nafasi ambayo inahitaji marekebisho ni safu ya ushambuliaji kwani imebainika wachezaji wao wamekua wakitengeneza nafasi nyingi, lakini wanashindwa kuzitumia vema kwa kufunga mabao.
“Tumeingia kambini tangu Jumapili (Machi 27) tukiwa tunafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo dhidi ya US Gendarmerie ambao kwetu ni muhimu kushinda ili tufuzu robo fainali.”
“Katika michezo iliyopita ambayo tumefungwa dhidi ya ASEC na RS Berkane, kuna baadhi ya makosa ambayo wachezaji wetu waliyafanya ambayo tumeanza kuyafanyia kazi baada ya kuanza kambi, Hivyo hatutaki kuona yakitokea tena katika mchezo huu kwa sababu tunahitaji kufikia malengo ya kuifi kisha timu robo fainali,” amesema Matola.
Simba SC ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi D, ikiwa na alama 07 sawa na RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya pili, huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiwa kileleni kwa kuwa na alama 09.
US Gendamarie ya Niger itakayocheza dhidi ya Simba SC Jumapili (April 03) inashika nafasi ya nne kwenye kundi hilo kwa kuwa na alama 05.