Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za Serikali kujiangalia upya na kufanya mabadiliko ya watendaji na ufanyaji kazi kwa ngazi zote.
Rais Samia amesema hayo, katika hafla ya kupokea taarifa ya Ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka 2022/221 pamoja na ripoti ya taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ikulu Chamwino.
Kati ya Taasisi ambazo amezitaja ni Bohari kuu ya Dawa MSD, ambapo amesema kuwa wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hasa katika kuhudumia soko la nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Rais Samia pia amezitaka taasisi nyingine zinazojihusisha na kukopa mikopo chechefu kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii kurejesha kwa wakati mikopo hiyo na kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko hiyo.
Aidha Rais Samia amezitaka taasisi zinazohusika katika kuwakamatana na kuwachunguza wahusika wa dawa za kulevya, kutowaachia kama hawajapata ushahidi wa kutosha na endapo wanapata ushahidi basi wahakikishe sheria inafata mkondo wake.
“Napata malalamiko, huyu mama sasa anatoa wauza unga nje waje watuharibie watoto wetu, Sasa nyie mliopeleka ndani wauza unga, sijui TAKUKURU, DPP, angalieni kama mna ushahidi wa kutosha endeleeni na kesi zao, na kama hamna ushahidi mliwapeleka kibabebabe angalieni nini mnaweza kufanya,” Rais Samia.
“Kumbukeni mimi ni mkuu wa nchi, lolote mnalofanya mwisho ni la Mkuu wa nchi na kasema watolewe sasa watoto wetu wanakuja kuharibika, lakini wanaosimamia hili eneo la dawa za Kulevya na wenyewe wakae makini, hao wauza unga mliowapeleka kama hamna ushahidi wa nini wanafanya, fuatilieni ili muwe makini nalo.” Amesema Rais Samia.
Rais Samia pia amempongeza Mkaguzi Mkuu na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuweza kupunguza kiwango cha hati chafu na kuweza kudhibiti usimamizi wa Rasilimali za Umma.