Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara SImba SC, Pablo Franco amesema wachezaji wake wako katika hali nzuri na wameahidi kujituma kwa ajili ya kufikia malengo ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Barabni Afrika.
Simba SC itashuka Dimbani (Uwanja wa Benjamin Mkapa) jijini Dar es salaam kesho Jumapili (April 03) kurusha karata yake ya mwisho katika hatua ya Makundi ya Michuano hiyo, kwa kucheza dhidi ya USGN kutoka Niger, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote, ili itinge hatua ya Robo Fainali.
Kocha Pablo amesema anafahamu ugumu watakaokutana nao katika mchezo huo lakini amewaondoa hofu mashabiki wa Simba SC kwa sababu hawatabweteka huku kila mchezaji akitarajia kutimiza ndoto ya kufanya vizuri.
“Tunafahamu mchezo huu ni mhimu sana kwetu kama Simba SC, ninawaona wachezaji wangu wakiwa tayari kwa mapambano kesho Jumapili (April 03), wamenihakikishia watacheza kwa moyo wote ili kufanikisha mpango wa ushindi tuliojiwekea.”
“Wapinzani wetu wana uwezo mkubwa kisoka na wao wanahitaji kushinda ili kutimiza malengo yao, lakini sisi hatua budi kuutenda haki Uwanja wetu wa nyumbani kama tulivyofanya katika michezo dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast na RS Berkane ya Morocco.” Amesema Kocha Pablo.
Simba SC inahitaji ushindi ili kufikisha alama 10 zitakazoivusha kutoka hatua ya makundi hadi Robo Fainali, kufuatia hivi sasa kuwa na alama 07 zinazoiweka katika nafasi ya tatu, sawa na RS Berkane ya Morocco.
ASEC Mimosas ya Ivory Coast in anaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama 09, huku USGN itakayocheza dhidi ya Simba SC kesho Jumapili (April 03), ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 05.