Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umesema maandalizi ya mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USGN kutoka Niger yamekamilika.
Simba SC itashuka Dimbani (Uwanja wa Benjamin Mkapa) jijini Dar es salaam kesho Jumapili (April 03) kurusha karata yake ya mwisho katika hatua ya Makundi ya Michuano hiyo, kwa kucheza dhidi ya USGN kutoka Niger, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote, ili itinge hatua ya Robo Fainali.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally, amesema taratibu zote za kuiandaa timu yao na kuelekea kwenye mchezo huo zimeshakamilisha na kinachosubiriwa ni hatua za mwisho kabla ya kipyenga kupulizwa kesho Jumapili (April 03) saa nne usiku.
Ahmed amesema wachezaji wao wapo katika hamasa kubwa kuelekea mchezo huo na Uongozi umeshajizatiti kwa kila hatua, ili kufanikisha matarajio ya ushindi ambao utawavusha na kuwapeleka kwenye hatua ya Robo Fainali.
Hata hivyo Ahmed amewataka Mashabiki wa Simba SC kuendelea kukata tiketi za mchezo huo ili kufanikisha lengo la kuzaja nafasi 35,000 ambazo zimetolewa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’,
“Kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa, hadi sasa kila hatua ya maandalizi imepigwa kwa asilimia karibu 98, mengine yaliyobaki ni taratibu za CAF ambazo zitakamilishwa na maafisa wao na wale wa TFF.”
“Tunapenda pia kuwaambia mashabiki wetu ukienda kununua jezi ya Simba dukani kwa Vunja Bei, utapewa na tiketi ya bure ya Sh. 3,000, hii tumeweka ili kuhakikisha tunaujaza uwanja siku ya Jumapili,” Ahmed alisema.
Simba SC inahitaji ushindi ili kufikisha alama 10 zitakazoivusha kutoka hatua ya makundi hadi Robo Fainali, kufuatia hivi sasa kuwa na alama 07 zinazoiweka katika nafasi ya tatu, sawa na RS Berkane ya Morocco.
ASEC Mimosas ya Ivory Coast in anaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama 09, huku USGN itakayocheza dhidi ya Simba SC kesho Jumapili (April 03), ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 05.