Uongozi wa Klabu ya Simba SC umemtangaza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye kuwa Mgeni Rasmi kwenye mchezo wao wa mwisho hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USGN ya Niger.
Simba SC itashuka Dimbani (Uwanja wa Benjamin Mkapa) jijini Dar es salaam kesho Jumapili (April 03) kurusha karata yake ya mwisho katika hatua ya Makundi ya Michuano hiyo, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote, ili itinge hatua ya Robo Fainali.
Simba SC wamemtangaza Waziri Nape kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wakiamini kiongozi huyo atakuwa shuhuda mzuri wa kukiona kikosi chao kikipambana na kupata matokeo chanya kama ilivyo kwenye matarajio yao.
“Mgeni rasmi kwenye mchezo wa kesho dhidi ya USGN atakuwa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye. #NguvuMoja” Imeeleza Taarifa iliyochapishwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC
Simba SC inahitaji ushindi ili kufikisha alama 10 zitakazoivusha kutoka hatua ya makundi hadi Robo Fainali, kufuatia hivi sasa kuwa na alama 07 zinazoiweka katika nafasi ya tatu, sawa na RS Berkane ya Morocco.
ASEC Mimosas ya Ivory Coast in anaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama 09, huku USGN itakayocheza dhidi ya Simba SC kesho Jumapili (April 03), ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 05.