Imethibitika kuwa Kocha wa Simba SC Franco Balo Martin aliutaka Uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha kikosi chake kinafanya mazoezi kwa siku mbili nyakati za usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kikosi cha Simba SC kimefanya mazoezi katika Uwanja huo, juzi Ijumaa (April Mosi) na jana Jumamosi (April 02), ili kujiandaa na mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USGN kutoka nchini Niger, ambao utapigwa leo Jumapili (April 03) Saa Nne Usiku.

Chanzo cha Habari hizi kutoka ndani ya klabu ya Simba SC kimeeleza kuwa: “Kocha Pablo aliomba katika siku mbili kabla ya mchezo husika wachezaji kufanya mazoezi katika muda sawa na mchezo husika jambo ambalo limefanyika kwa ufasaha mkubwa, hivi sasa kikosi kipo tayari kwa mapambano.”

“Nia na mahitaji yetu ni kupata ushindi ili kutinga hatua inayofuata ya michuano hii, hivyo lazima tujue nini tunafanya kwa wakati sahihi na tusiwe nje ya mifumo itakayotupa matokeo.” Kimesema chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya klabu ya Simba SC.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, michezo yote ya mwisho ya Kundi D, itacheza muda sawa ili kuepuka mazingira ya kupanga matokeo.

Wakati Simba wakicheza na US Gendarmerie saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kule Morocco kwao itakuwa saa 2 usiku ambapo kutakuwa na mchezo kati ya RS Berkane dhidi ya ASEC Mimosas.

Simba SC inahitaji kushinda dhidi ya USGN ili ifikishe alama 10, zitakazoivusha kwenda Robo Fainali, huku Mshiriki mwingine kutoka Kundi D, katika hatua hiyo akitarajiwa kupatikana baada ya mchezo wa RS Berkane ya Morocco itakayokua nyumbani dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Msimamo wa Kundi D unaonyesha ASEC Mimosas inaongoza ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane yenye alama 07 sawa na Simba SC, huku USGN ikiburuza mkia kwa kufikisha alama 05.

Khalid Aucho hatarini kuikosa Azam FC
Dkt. Mabula: Wanachi washilikishwe maamuzi Baraza la Mawaziri