Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na klabu ya Simba SC Bernard Morrisson amewashukuru Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo waliojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa jana Jumapili (April 03).
Simba SC ilicheza mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USGN ya Niger, kuanzia saa nne usiku, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mabingwa hao wa Soka Tanzania Bara kucheza muda huo ikiwa nyumbani Dar es salaam.
Morrison ambaye alianza kwenye kikosi cha Simba SC na kufanikiwa kutoa pasi mbili za mwisho zilizozaa mabao, ametoa shukurani hizo kwa kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram.
Ujumbe huo wa Morrison emeonyesha Mashabiki na Wanachama waliojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa walikua chachu kwa timu yao kufanya vizuri na kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
“Tulihitaji sapoti yenu dakika za mwisho usiku wa jana na mkafanya zaidi ya ilivyotarajiwa, mlichokifanya ninyi mashabiki usiku wa jana ni upendo wa hali ya juu. Mtoto wangu ajae ataitwa ‘Mashabiki Wa Simba Morrison.” ameandika Morrison
Simba SC iliibuka na ushindi wa 4-0 na kutinga Robo Fainali kwa kufikisha alama 10 zilizoiweka nafasi ya pili kwenye Msimamo wa ‘Kundi D’ sawa na RS Berkane iliyoshinda nyumbani 1-0 dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Mabao ya Simba SC yalifungwa na Sadio Kanoute na Chriss Mugalu aliyefunga mabao mawili huku Mlinda Lango wa USGN Saidou Hamisu akijifunga baada ya kushindwa kuutuliza mpira wa kurudishiwa na beki wake.