Beki wa Kushoto na Nahodha Msaidizi wa Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amebeba jukumu la kutoa shukuruni kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kwa niaba ya wachezaji wenzake.
‘Tshabalala’ ametoa shukurani hizo baada ya kutimiza lengo la kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga USGN ya Niger 4-0.
Beki huyo ambaye jana hakumaliza mchezo kufuatia majeraha ya mguu yaliyomkabili amesema: “Kwa niaba ya wachezaji wote wa Simba SC napenda kutoa shukrani kwa mashabiki wote na watanzania kwa ujumla mliojitokeza jana Mungu awabariki hakika ulikuwa Usiku mzuri sana”
Simba SC inasuburi Droo ya Robo Fainali itakayopangwa kesho Makao Makuu ya Shirikisho Barani Afrika Cairo-Misri, huku akitarajia kukutana na timu zilizomaliza nafasi ya kwanza katika Kundi A. B na C.
Al Ahly Tripoli ya Libya ndio Kinara wa Kundi A, Olarndo Pirates ya Afrika Kusini wamemaliza kinara wa kundi B na Kundi C linaongozwa na TP Mazembe ya DR Congo.
Timu zilizomaliza katika nafasi ya pili kwenye kila Kundi ikiwemo Simba SC, zitaanzia nyumbani kucheza Robo Fainali ya Mkondo wa Kwanza kisha itamalizia Ugenini Kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili.
Michezo ya Mkondo wa kwanza imepangwa kuchezwa kati ya April 15-17, huku Michezo ya Mkondo wa pili ikitarajiwa kuchezwa kati ya April 22-24.
Hafla ya Kupanga michezo ya Hatua ya Robo Fainali inatarajiwa kufanyika Kesho Jumanne (April 05) Mjini Cairo nchini Misri saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki.