Ndugu na watu wa karibu wa Mwanamuziki wa rap kutoka nchini Marekani Markelle Morrow maarufu Goonew wameibua gumzo kote duniani baada ya kuupeleka mwili wa rapa huyo kwenye klabu ya usiku na kisha kuusimamisha mbele ya idadi kubwa ya watu.
Ndugu hao wamedai kuwa ni tukio maalum la kumuaga na kumpa heshima za mwisho ndugu yao na kusherehekea maisha ya rapa huyo.
Kinyume cha matarajio ya wengi, mwili wa rapa huyo uliingizwa katika klabu ya usiku ambapo muziki ulikuwa ukirindima huku kundi kubwa la watu waliohudhuria wakionesha kusherehekea wakiimba kwa furaha.
Maiti ya mwanamuziki huyo ilisimamishwa kwenye jukwaa ikiwa imeshikizwa kwenye ukuta ikiwa imevalia mavazi mithili ya mtu aliye hai.
Kufuatia tukio hilo la kustaajabisha maelfu ya watu wamekuwa na mitazamo ya tofauti juu ya tukio hilo, huku watu wa karibu wa rapa huyo wakidokeza kuwa suala hilo ni sehemu ya kutekeleza akichokiomba marehemu mwenyewe enzi za uhai wake kuwa afanyiwe hivyo atakapokuwa amekufa.
Kwa mujibu wa ripoti za TMZ inaelezwa kuwa bado uchunguzi unafanyika kubaini ukweli wa jambo hilo ikiwa ulitumika mwili halisi wa marehemu Goonew
Goonew aliuawa kwa kupigwa risasi huko District Height Maryland, Machi 28, 2022.