Siku Moja baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kupanga Droo ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho, huku Simba SC ikiangukia mikononi mwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Uongozi wa klabu hiyo umesema umeanza maandalizi kuelekea mchezo huo ambao utapigwa kati ya April 15-17, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Simba SC itaanzia nyumbani kisha itakwenda Afrika Kusini kucheza mchezo wa mkondo wa pili kati ya April 22-24.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu ya Simba SC Ahmed Ally amesema wanaiheshimu Orlando Pirates kutokana na ukubwa wake katika soka la Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla, na hawana budi kuanza maandalizi mara moja kuelekea mchezo huo.
Amesema kitendo cha klabu hiyo kutinga Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho, ni dhahir kinaonyesha ni klabu kubwa na ilistahili kuwa hapo ilipo, hivyo Simba SC imepokea kwa mikono miwili Droo ya ‘CAF’ na imeanza kujipanga.
“Ni klabu kubwa pale Afrika Kusini, ni Klabu Kubwa pale Soweto, huwezi kumchukulia poa mtu aliyetinga Robo Fainali, kuna vitu amevifanya huko na ndio maana ametinga katika hatua hii, tunakwenda kukutana wakubwa ambao tunajua uchungu na thamni ya Michuano hii.”
“Mchezo huu ni vita kati ya Vijana wa Julius Nyerere na Nelson Mandela, itakua vita ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Damu itamwagika Uwanja wa Benjamin Mkapa, hatma ya Simba SC kutinga Nusu Fainali ipo mikononi mwa Simba SC yenyewe, haiko mikononi mwa Orlando Pirates.”
“Kama tukizichanga vizuri karata zetu, tuna uhakika kabisa wa kutinga Nusu Fainali, Orlando pamoja na ukubwa wake niliokwambia na sifa zake nilizozitaja, hawana uwezo wa kumzuia Mnyama kutinga Nusu Fainali.
“Ninaamini tukicheza vizuri mchezo wetu wa Mkondo wa Kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa, tuna uhakika wa asilimia 100 wa kufanya vizuri katika mchezo huo, na mchezo wa marudiano utakua mchezo wa kula Tende na Kahawa, kwa hiyo ninarudia hatma ya Simba SC kutinga Nusu Fainali ipo mikononi mwa Simba SC yenyewe, haiko mikononi mwa Orlando Pirates.” amesema Ahmed Ally.
Simba SC ilitinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho kwa kishindo Jumapili (April 03), kwa kuichapa USGN ya Niger mabao 4-0, na kufikisha alama 10 kwenye msimamo wa Kundi D, huku ikishika nafasi ya pili ikitanguliwa na RS Berkane ya Morocco iliyomaliza kinara wa Kundi hilo.