Kocha Mkuu wa Coastal Union ya Tanga Juma Mgunda amefunguka kuelekea mchezo wa Kesho Alhamis (April 07) wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utashuhudia kikosi chake kikicheza dhidi ya Mabingwa watetezi Simba SC, Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Mgunda atakua shuhuda wa mchezo huo kwa mara ya kwanza tangu aliporejeshewa jukumu la kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la klabu hiyo ambaye aliwahi kuitumikia kama Mchezaji enzi za ujana wake.

Kocha huyo Mzawa amesema anatarajia mchezo wenye ufundi wa hali ya juu, kutokana na Simba SC kuwa na kikosi imara na chenye hitaji la kusaka ushindi, hivyo amejipanga kukabiliana na timu hiyo kutoka Dar es salaam.

Amesema jukumu kubwa lililo mbele yake ni kuhakikisha Coastal Union inapambana katika Uwanja wake wa nyumbani Kesho Alhamis (April 07) na kupata matokeo chanya, ambayo yanasubiriwa na Mashabiki wa soka Jijini Tanga.

“Utakua mchezo wa ufundi sana, na mimi nimekiandaa kikosi changu katika mipango ya kiufundi ili tuikabili vizuri Simba SC, ninajua wapinzani wetu wanahitaji kubwa la kusaka ushindi kama walivyofanya katika michezo yao huko nyuma, lakini niwatoe hofu Mashabiki wa Coastal Union kwa kusema kikosi changu kipo vizuri na kimejiandaa vyema.”

“Hapa ninamaanisha hivi, Kiufundi Fundi anapokutana na Fundi, lazima ujiandae kwa Ufundi, ndivyo nilivyokiandaa kikosi changu kitakachoivaa Simba SC kesho Alhamis.” Amesema Juma Mgunda.

Tayari Simba SC imewashawasili Jijini Tanga tangu jana Jumanne (April 05) na leo Jumatano (April 06) imefanya maandalizi yake ya mwisho katika Uwanja wa CCM Mkwakwani kuelekea mchezo dhidi ya Coastal Union kesho Alhamis (April 07).

Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 37 baada ya kucheza michezo 16, huku Coastal Union iliyocheza michezo 18 hadi sasa, ikiwa nafasi ya 11 kwa kumiliki alama 21.

Mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22, timu hizo zilipokutana Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, timu hizo zilitoka sare ya 0-0.

Pablo Kocha Bora Ligi Kuu Tanzania Bara
Ahmed Ally: Hatma ya Simba Kucheza Nusu Fainali ipo kwa Simba yenyewe