Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba SC Pablo Franco Martin ametajwa kuwa Mshindi wa Tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Pablo ametajwa kuwa Mshindi wa Tuzo hiyo, kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ leo Jumatano (April 06), huku akikamilisha maandalizi ya mwisho ya kikosi chake kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga utakaopigwa Kesho Alhamis (April 07).
Taarifa ya TPLB imeeleza kuwa, Kocha Pablo ambaye ni Raia wa Hispania ametajwa kuwa Mshindi, akiwashinda Makocha Nasreddine Nabi wa Young Africans na Fred Felix Minziro wa Geita Gold FC.
Kocha Pablo alikiongoza vizuri kikosi chake kushinda michezo dhidi ya Biashara United Mara kwa mabao 3-0, Kisha akaiburuza Dodoma Jiji FC mabao 2-0.